SERA YA MIKOPO 


   UTANGULIZI

Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo VIWANGO SACCOS LTD. kilianzishwa na wafanyakazi wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) tarehe 28.04.1986 na kusajiliwa kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Ushirika Na. 15 ya mwaka 1982 ambayo ilifanyiwa maboresho mwaka 1991 na kupewa namba ya usajili PRI-DAR-UBG-MC-2022-1022 na leseni namba MSP3-TCDC/2022-00089.

 

Sera hii ya mikopo imeandaliwa ili kuweka wazi taratibu za ukopeshaji mikopo kwa wanachama.Vilevile kutoa huduma ya kuweka akiba za kifedha na kupata mikopo wakati inapohitajika.

 

 MADHUMUNI YA SERA YA MIKOPO YA VIWANGO SACCOS LTD

Madhumuni ya sera ni:

(a)    kumuwezesha mwanachama kujua taratibu za ukopeshaji na nyaraka zinazohusika.

(b)    kumuwezesha mwanachama kujua masharti ya kukidhi kupata mkopo.

(c)    kumuwezesha mwanachama kujua aina za mikopo na dhamana zinazokubalika

(d)    kumuwezesha mwanachama kujua ukomo wa mikopo ikijumuisha kiwango cha juu cha mkopo kwa mkopaji.

(e) kumuwezesha mwanachama kujua adhabu au ada kwa marejesho yaliyocheleweshwa;

(f)     kumuwezesha mwanachama kujua vigezo na masharti ya mkopo kama viwango vya riba, ada, tozo na idadi ya marejesho.

(g)    kuiwezesha viwango SACCOS kufanya tathimini ya uwezo wa mkopaji kurejesha mkopo.

(h)  kuisaidia kamati ya mikopo kujua ukomo wa juu wa uidhinishaji mikopo.

(i)      Kumuwezesha mwanachama kujua masharti ya udhamini wa mkopo

(j)       Kumsaidia mwanachama kujua kipindi kinachotolewa kabla ya kuanza kurejesha mkopo

(k)    kuiwezesha Viwango SACCOS kuweka utaratibu wa ukusanyaji na ufuatiliaji wa mikopo.

(l)      kuiwezesha Viwango SACCOS kuweka vigezo na taratibu za kurekebisha masharti ya mikopo na uhamishaji wa hisa za hiari za mwanachama ikijumuisha idhini na ruhusa

(m)  kuiwezesha Viwango SACCOS kuweka kigezo na taratibu za kuidhinisha na kuruhusu kufuta mikopo isiyolipika ufuatiliaji na tathimini ya ubora wa mikopo

(n)    kumuwezesha mwachama kujua fomu husika zinazotumika kwa ajili ya maombi ya mkopo

(o)    kupunguza hatari ya mikopo mibaya

(p)    kujenga imani kwa taasisi za ndani na nje, wanachama na wananchi kwa ujumla.

(q)    kuonyesha umakini wa Bodi katika kusimamia shughuli za chama

 

 

 WALENGWA WA SERA

Walengwa wakuu katika sera hii ni wanachama na watendaji wa VIWANGO SACCOS ambapo Mwanachama mmoja mmoja hukopa kulingana na mahitaji yake na uwezo wake wa kulipa baada ya kuwasilisha fomu  ya maombi ya mkopo husika.

 

 MISINGI NA UTARATIBU WA UTOAJI MIKOPO

  Misingi ya utoaji wa mikopo kwa wanachama:

 

a)    MTAJI (CAPITAL)

Akiba za wanachama zilizowekwa ndani ya chama zitazingatiwa na kuwa kigezo muhimu cha kutoa mkopo kwa mwanachama.

 

b) TABIA (CHARACTER)

Tabia ya mkopaji lazima itathiminiwe kulingana na uaminifu wake binafsi na kumbukumbu zake za mikopo. Wanachama, kamati ya usimamizi, kamati ya mikopo au kiongozi yeyote wa chama anayemfahamu mkopaji anaweza kutoa tathimini ya tabia yake katika kurejesha mikopo. Dhamana kubwa iliyopita kiwango cha mkopo isiwe kigezo cha kumpa mkopo mwanachama asiyekuwa na tabia nzuri ya urejeshaji. Wakopaji wapya watatathiminiwa kwa kuzingatia uwezo wao wa akiba/dhamana.

 

c)   HALI (CONDITION)

Hali ya utoaji wa mkopo kwa mwanachama itazingatia mambo ya nje yanayoathiri mkopo wa mwombaji ambayo ni: hali ya uchumi wa nchi, thamani ya fedha, sheria za nchi, hali ya soko la kazi/ajira na mambo mengine yanayoathiri hali ya urejeshaji wa mkopo

 

d) UWEZO WA MTIRIRIKO WA KIFEDHA (CAPACITY)

Uwezo wa kurejesha mkopo ndiyo kitu cha kwanza cha msingi cha kuangalia katika kutathimini uwezo wa mwanachama kurejesha mkopo anaoomba, katika kuchanganua uwezo wa kurejesha mkopo, vitu vitatu vitazingatiwa:

                      i.        Uwezo wa kurejesha mkopo

                     ii.        Uwezo na matarajio ya kupata marejesho

                    iii.        Hali ya kifedha

 

e)   DHAMANA (COLLATERAL)

                      i.        Dhamana ya kwanza ya mkopo itakuwa ni Akiba, Hisa na Amana za mwanachama husika.

                    ii.        Mwanachama yoyote aliyetimiza mwaka mmoja tangu kujiunga kwake anaweza kumdhamini mwanachama mwenzake pindi achukuapo mkopo,

 

f) WADHAMINI

Endapo mkopaji atashindwa kulipa deni lake, mdhamini/wadhamini atawajibika kulipa deni la mkopo huo ikiwa ni pamoja na kuzuia akiba, hisa na amana zake chamani.

 

 UTARATIBU WA UTOAJI MIKOPO

1 Mwanachama anayekusudia kupata mkopo atawasilisha maombi kwa kutumia fomu maalum iliyoandaliwa na              VIWANGO SACCOS

 

2 viwango SACCOS Itatoa mikopo isiyozidi miezi 48 kwa ajili ya kuweka mzunguko endelevu wa fedha.

 

3 Mwanachama mpya ambaye hajathibitishwa kazini atakuwa na haki ya kukopa mkopo wa dharura, Elimu na maalum pekee kulingana na uwezo wake wa kulipa.

 

4 Mwanachama mpya aliyethibitishwa kazini, pamoja na mikopo mingine atakuwa na haki ya

      kukopa hadi mara mbili ya akiba zake kwa mkopo wa maendeleo na mkopo wa gari kulingana

      na uwezo wake wa kulipa.

5 Mwanachama aliyethibitishwa kazini na aliyemaliza kulipa mkopo wa maendeleo na mkopo

      wa gari awamu ya kwanza kikamilifu atakuwa na haki ya kukopa hadi mara tatu ya akiba zake

      kwa mkopo wa maendeleo na mkopo wa gari kulingana na uwezo wake wa kulipa.

 

6 Maombi ya mikopo ya Maendeleo, ujasiriamali na gari kwa hatua za mwanzo yatapitiwa na

      Meneja/Afisa mikopo wa chama na kupelekwa kwenye kikao cha kamati ya Mikopo kwa hatua

      ya mwisho ya kujadiliwa na kuidhinishwa.

 

7 Maombi ya mikopo ya Dharura, maalum na elimu yatapitiwa na kuidhinishwa na Meneja/Afisa

      mikopo wa chama na kuwasilishwa kwa Karani wa mahesabu kwa hatua ya malipo.

 

8 Mikopo ya Maendeleo na gari itapitishwa na kikao cha kamati ya Mikopo kutegemeana na     

      upatikanaji wa fedha,

 

9 Maombi ya mikopo yatafuata utaratibu wa “aliyekuja kwanza kupewa kwanza” (First come

      first served basis).

 

10 Ikitokea maombi ya mikopo yanazidi kiasi cha fedha zilizopo, kipaumbele kitatolewa kwa

        maombi yenye kiasi kidogo, hata hivyo wakati maombi ya mikopo yatakapojadiliwa hatua

        zifuatazo zitafuatwa/ kuzingatiwa

 

a.    Mwanachama ambaye ni mara yake ya kwanza kuomba mkopo

b.    Mwanachama ambaye amemaliza kulipa mkopo uliotangulia bila matatizo na kuomba mkopo mwingine

c.    Mwanachama ambaye ameshalipa nusu ya mkopo wa awali

 

11 Maombi ya mkopo yakiidhinishwa fomu ya mkopo itasainiwa na kuonyesha mpango wa

      ulipaji (Repayment schedule) pamoja na mkataba wa ukopaji mkopo kati ya mwanachama na      

      chama. Baada ya hapo malipo yatafanyika kwa hundi au kuhamishwa moja kwa moja kwenye

      akaunti ya mkopaji.

 

 RIBA

Viwango vya riba vitapendekezwa na Bodi na kuidhinishwa na Mkutano Mkuu. Mabadiliko ya riba hayataathiri Mikopo iliyotolewa kabla ya mabadiliko.

 

 KINGA DHIDI YA MAJANGA (BIMA YA MIKOPO)

1 Mkopo wa Maendeleo, Mkopo wa gari, mkopo maalum, na mkopo wa dharura utakaotolewa

   kwa mkopaji, utalipiwa bima ya asilimia moja (1%) ya kiwango cha mkopo kilichoidhinishwa.

 

2 Endapo mwanachama atapata ulemavu wa kutojiweza au kufariki, kinga dhidi ya majanga italipa mkopo uliobakia. Akiba, hisa na amana za mwanachama husika zitakabidhiwa kwake mwenyewe au kwa familia/msimamizi wa mirathi wa marehemu.

 

 TOZO LA ADHABU

Rejesho litakalocheleweshwa kwa zaidi ya siku thelathini (30) litatozwa tozo la adhabu ya asilimia tano (5%) kwa kila mwezi unaozidi makubaliano ya marejesho

 

 MASHARTI YA UJUMLA YA UTOAJI WA MKOPO

1 Mkopo utatolewa kwa mwanachama hai wa viwango SACCOS Ltd (aliyetoa kiingilio, aliyenunua

   hisa kamili na kuweka akiba ya lazima kila mwezi na kuwa ndani ya viwango SACCOS Ltd kwa

   muda usiopungua miezi mitatu toka alipojiunga na chama.

 

2  Maombi ya mikopo ya Maendeleo na gari ni lazima yaletwe mwezi mmoja kabla.

 

3  Mikopo ya dharura, elimu na maalum itatolewa siku yoyote ya kazi itakapohitajika

 

4  Mkopo wowote utakaotolewa kabla ya tarehe 15, marejesho yake yataanza mwezi   huohuo na mikopo itakayotolewa baada ya tarehe 15 marejesho yake yataanza mwezi unaofuata.

 

5 Maombi ya mikopo ya Maendeleo na Gari yatajadiliwa katika vikao halali vitakavyofanywa na kamati ya mikopo ya viwango SACCOS Ltd kwa Quorum inayotakiwa.

 

6 Kamati ya mikopo itachukua hatua ya kutoidhinisha mkopo ulioombwa hadi hapo masharti yatakapotimia au kuomba taarifa za nyongeza kutoka kwa mwanachama, mwajiri n.k

 

7  Endapo maombi ya mkopo yamekataliwa au hayakuidhinishwa muombaji atafahamishwa kwa maandishi sababu za kukataa maombi hayo ndani ya siku saba baada ya kikao cha kamati ya mikopo kumalizika.

 

 

AINA ZA MIKOPO NA MAREJESHO YAKE

1 MKOPO WA MAENDELEO

Mkopo huu utatolewa kulingana na akiba za mwanachama na utakopeshwa kwa madhumuni ya kufanikisha shughuli za kimaendeleo

 

 

2 MKOPO WA GARI

Mkopo huu utatolewa kulingana na akiba za mwanachama na utakopeshwa kwa madhumuni ya kufanikisha ununuaji wa gari

 

 

3 MKOPO MAALUM

 

4 MKOPO WA DHARURA

 

5 MKOPO WA ELIMU

 

 UFUATILIAJI WA MIKOPO NA MATENGO YA MIKOPO MIBAYA

 

1 KUREJESHA MKOPO

 

2 MIKOPO/MADENI MABAYA

1.    Iwapo malipo ya marejesho ya mwanachama yatakuwa pungufu ya malipo yaliyotakiwa kulipwa kwa mujibu wa masharti ya mkataba uliosainiwa na mwanachama kipindi anapochukua mkopo

2.    Endapo malipo ya marejesho ya mwanachama hayatafanyika ndani ya siku thelathini tangu marejesho hayo kutakiwa kufanyika bila kujali kuwa mkopo uliocheleweshwa ni riba tu au riba na mkopo

3.    Iwapo jedwali la marejesho ya mkopo lililopo kwenye fomu ya mikopo halitazingatiwa katika marejesho ya mkopo ya mwanachama

4.    Chama kitatayarisha taarifa ya mikopo iliyocheleweshwa ndani ya siku kumi na tano (15) baada ya kuisha kipindi ambacho taarifa hiyo inahusika. Taarifa ya ucheleweshwaji wa mikopo itajumuisha mambo yafuatayo:

                                           i.        Jina la mwanachama, anwani yake binafsi

                                         ii.        Mkopo halisi uliotolewa na baki ya deni linalodaiwa

                                        iii.        Majina ya wadhamini na dhamana yake

                                        iv.        Taarifa nyingine zinazohusika kwa mujibu wa fomu ya mkopo

 

3 UKOKOTOAJI NA UAINISHAJI MIKOPO ILIYOCHELEWESHWA

     Chama kitakuwa kinafanya ukokotoaji wa mikopo iliyocheleweshwa kwa kuanzia tarehe ya

     mwisho ambayo rejesho la mkopo husika lilifanyika mpaka pale yatakapokuwa yamekamilika.

     Mikopo iliyocheleweshwa itakokotolewa kila mwezi na kutolewa taarifa siku ya mwisho wa

     mwezi ambapo mikopo hiyo itaainishwa katika makundi yafuatayo:

 

·         Mikopo iliyopo kwenye angalizo-kuchelewa kwa siku 31-90

·         Mikopo iliyopo chini ya kiwango-kuchelewa siku 91-180

·         Mikopo yenye mashaka-kuchelewa ni siku 181-365

 

 HITIMISHO

11.1      VIWANGO SACCOS inaongozwa kwa kuzingatia sheria ya vyama vya ushirika    no 06 ya mwaka 2013 na kanuni zake za mwaka 2015 pamoja na sheria no 10 ya asasi ndogo za fedha ya mwaka 2018 na kanuni zake za mwaka 2019 na miongozo mbalimbali ya Mrajis, masharti ya chama na sera mbalimbali za chama.

 

11.2      Wanachama wa VIWANGO SACCOS ndiyo walinzi wa taratibu zilizotajwa hapo juu kwa kuzingatia sheria, kuwa wakweli na kutekeleza wajibu wao ili kuboresha huduma za chama.

 

11.3      Haki ya kukopa aliyonayo mwanachama iendane na wajibu wa kuilinda sera hii ili iwe mwongozo wa shughuli za chama

 

UTHIBITISHO

Sera hii imethibitishwa, kusomwa, kujadiliwa na kukubaliwa na Mkutano Mkuu wa Wanachama wote wa Viwango SACCOS uliofanyika tarehe 09-12-2023

 

KAULI MBIU: KOPA KWA BUSARA LIPA KWA WAKATI